Evans Wadongo

Evans Wadongo (amezaliwa 11 Machi 1986) ni mhandisi kutoka nchini Kenya, mwenyekiti wa chama kisicho cha serikali "Sustainable Development For All-Kenya (SDFA-Kenya)" na mvumbuzi wa taa ya solar kwa ajili ya watu wanaoishi mashambani bila umeme.

Evans Wadongo alizaliwa kama mtoto wa wazazi walimu katika wilaya ya Kakamega, Kenya. Alisoma shule ya msingi Bisunu akaendelea baadaye kwenye sekondari ya Kakamega High School alipomaliza kati ya wanafunzi bora wa Kenya akishika wastani ya A kwenye Kenya Certificate of Secondary Education mwaka 2002. Akajiunga na Jomo Kenyatta University of Agriculture and Technology akamaliza mwaka 2009 kama bachelor of science.

Alipokuwa mwanafunzi alivumbua 2004 taa ya solar aliyoita "MwangaBora" akiwaza matumizi ya nishati ya jua kuwa njia njema ya kuhifadhi mazingira, kupunguza kukatwa kwa miti na kuboresha maisha ya watu mashambani wanaoishi katika mazingira pasipo na umeme jinsi ilivyokuwa katika kijiji chake wakati alipokuwa mtoto mwenyewe. Hakuvumbua taa za solar lakini alitumia teknolojia iliyokuwepo katika nchi zilizoendelea na kuilinganisha na mazingira ya Kenya. Pamoja na wengine aliunda chama kisicho cha serikali Sustainable Development For All-Kenya (SDFA-Kenya) kilichoendelea kusambaza wazo la kutumia nishati ya jua kwa kuboresha maisha ya watu. Taa ya solar inatengenzwa kwa bei nafuu na wafundi Wakenya kwa kutumia mabaki ya metali kutoka viwandani na karahana na diodi za LED zinazotumia umeme kidogo.

Mwaka 2010 shirika la habari la CNN ilitambua sifa zake kwa kumpatia cheo cha "Mshujaa wa CNN" katika ya chaguo la "top ten heroes of 2010". Mwaka 2011 alikabidhiwa tuzo la mfuko wa Mikhail Gorbachev kwa "watu waliobadilisha dunia".

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]