Koigi Wamwere

Koigi Wamwere ni mwanasiasa, mwanaharakati, na mwandishi kutoka nchi ya Kenya. Koigi alizaliwa mwaka wa 1949 huko Bahati, wilaya ya Nakuru. Koigi anajulikana kwa kujaribu kupindua serikali za Jomo Kenyatta na Daniel arap Moi. Koigi aliwekwa kizuizini na watawala hawa, na baadaye alikimbilia uhamishoni nchini Norway miaka ya 80. Baada ya kurudi Kenya miaka ya 90, Koigi alikamatwa na kushtakiwa kwa madai ya kuhusika na uhaini na uporaji kwa kutumia silaha. Kutokana na kampeni kubwa ya kimataifa dhidi ya kesi hiyo ambayo ilichukuliwa kuwa na nia ya kumnyamazisha, serikali ya Kenya ilimwachia huru.

Koigi ni mwandishi wa vitabu na makala kadhaa. Vitabu vyake ni "A Woman Reborn", "Justice on Trial", na "I Refuse to Die".

Hivi sasa Koigi ni mbunge wa jimbo la Subukia na waziri msaidizi wa Habari katika serikali ya Mwai Kibaki. Koigi, ambaye huko nyuma alikuwa na nywele msokoto (dreadlocks), alinyoa nywele zake baada ya kuangushwa kwa serikali ya chama cha KANU kutimiza ahadi yake kuwa atanyoa nywele baada ya ushindi dhidi ya chama hicho kupatikana.