Mazingira ya Yesu

Mfululizo wa kurasa juu ya Yesu
Yesu
Yesu Kristo na Ukristo

Umwilisho  • Utoto wa Yesu  • Ubatizo
Arusi ya Kana • Utume wa Yesu • Mifano ya Yesu  • Miujiza ya Yesu
Kugeuka sura • Karamu ya mwisho • Msalaba wa Yesu  • Maneno saba
Kifo cha Yesu  • Ufufuko wa Yesu
Kupaa mbinguni  • Ujio wa pili
Injili  • Majina ya Yesu katika Agano Jipya  • Yesu kadiri ya historia  • Tarehe za maisha ya Yesu • Kristolojia

Mazingira ya Yesu

Wayahudi • Kiaramu • Bikira Maria • Yosefu (mume wa Maria) • Familia takatifu • Ukoo wa Yesu • Ndugu wa Yesu • Yohane Mbatizaji

Mitazamo juu ya Yesu

Mitazamo katika Agano Jipya · Mitazamo ya Kikristo • Mitazamo ya Kiyahudi • Mitazamo ya Kiislamu • Yesu katika sanaa

Mto Yordani unaotiririka kutoka Syria hadi Bahari ya Kifo ukiwa karibu wote chini ya usawa wa bahari.
Hekalu la Yerusalemu linavyofikiriwa kuwa wakati wa Yesu.

Mazingira ya Yesu ni jumla ya mambo ya kijiografia na ya kihistoria yaliotangulia au kuendana na maisha ya Yesu Kristo, akimuathiri kama binadamu katika namna yake ya kuwaza, kusema na kutenda.

Ni muhimu kuyajua ili kumuelewa zaidi mwenyewe, kazi yake na ujumbe wake.

Jiografia na historia ya awali

[hariri | hariri chanzo]

Nchi ambayo Yesu alizaliwa akafundisha ni nchi ileile ambayo Mungu aliwaahidia Waisraeli tangu zamani za Abrahamu, ni nchi ileile waliyoiteka chini ya Yoshua, ni nchi ileile waliyoirudia kutoka utumwani Babeli. Awali ilikuwa sehemu ya Kanaani, baadaye ikaitwa Israeli na hatimaye Palestina kutokana na Wafilisti waliokuwa wameteka sehemu ya pwani kusini karibu wakati uleule wa Waisraeli kuteka sehemu kubwa ya nchi wakitokwa Misri (karne ya 13 KK).

Historia ya jirani

[hariri | hariri chanzo]

Katika karne ya 2 KK Wayahudi, walipodhulumiwa na Antioko Epifane ili waasi dini yao, walianza kupigania uhuru wao wa kidini na wa kisiasa chini ya ukoo wa Wamakabayo, ambao kwa imani na ushujaa mkubwa wakafaulu kushinda majeshi ya kutisha (1Mak 3:18-22), kutakasa hekalu (1Mak 4:36-61) na kurudisha ufalme wa Israeli mpaka baada ya Warumi kuweka Uyahudi chini ya himaya yao (63 K.K.).

Madhehebu na hali ya imani

[hariri | hariri chanzo]

Matukio hayo ndiyo asili ya kundi la Mafarisayo (yaani “waliojitenga”), walioshika kwa bidii Torati kadiri ya mapokeo ya walimu wa sheria, wengi wao wakiwa walei. Kwa jumla walileta uamsho wa kiroho kati ya Wayahudi, lakini walidharau wenzao wasiojua Biblia ya Kiebrania.

Pia walishindana sana na Masadukayo kuhusu masuala ya dini na ya siasa hata kusababisha mauaji; kwa kuwa Masadukayo (waliokuwa na nguvu kati ya makuhani) walikataa mafundisho hayo mapya huku wakishika Torati tu.

Baada ya Torati kuzidi kuzingatiwa na Wayahudi, wataalamu wake pia walizidi kuheshimiwa kama watu wa Neno la Mungu, wanaoleta mwanga wake katika maisha ya jamii.

Hekima, iliyotafutwa hasa chini ya Wagiriki, ilipotambulika kuwa inapatikana katika Torati, wataalamu hao wakaja kushika nafasi ya watu wa hekima kama vile hao walivyoziba pengo lililoachwa na manabii.

Wayahudi walizoea hali hiyo kiasi kwamba wakaona vigumu kumkubali Yesu ambaye hafafanui Torati kwa kufuata mapokeo ya wataalamu, bali kwa kujiamini kama manabii waliojiona wabebaji wa Neno la Mungu.

Alijitangaza kuwa ndiye Hekima ya milele ambaye ndani yake tunamjua Mungu, hivyo mwenendo wake na mafundisho yake haviwezi kuishia mambo yaliyozoeleka, kwa sababu kila mara ya Mungu yanapindua ya binadamu. La kufanya ni kujitahidi kufuata, halafu kuelewa: ndiyo wongofu ambao Yesu aliudai pamoja na imani.

Utawala wakati wa Yesu

[hariri | hariri chanzo]

Lakini wakati wote wa Agano Jipya, yaani tangu Yesu alipozaliwa hadi mwisho wa maisha ya mitume wake, nchi hiyo haikuwa huru, bali chini ya himaya ya Warumi, ingawa pengine hao waliwakabidhi vibaraka, yaani watawala wenyeji waliowekwa na wakoloni.

Vibaraka hao ni Herode Mkuu (37-4 K.K.) na wazawa wake, ambao tena hawakuwa Waisraeli halisi bali Waedomu ingawa kabila lao lililazimishwa kuingia dini ya Uyahudi karne iliyotangulia. Ukoo huo unajulikana kwa ukatili, uchu wa madaraka na uzinifu wake.

Vilevile maliwali wa Kirumi waliowekwa pengine kutawala nchi au sehemu fulani walionyesha mara nyingi ukatili na dharau kwa Waisraeli na dini yao, hata kusababisha chuki na mapigano kati ya jeshi lao na wananchi. Mfano mmojawapo ni Ponsyo Pilato aliyesimamia Uyahudi kuanzia mwaka 26 hadi 36 B.K.

Mbali na hayo, utawala wa Roma, ulioenea Ulaya Magharibi na Kusini, Afrika Kaskazini na nchi za Mashariki ya Kati kupakana na Iraq ya leo, kwa jumla ulihakikisha hali ya amani kwa muda wote wa Agano Jipya na karne za kwanza za Kanisa.

Manufaa ya hali iliyokuwepo

[hariri | hariri chanzo]

Hali hiyo, pamoja na umoja wa dola hilo lote, na urahisi wa mawasiliano kwa njia ya barabara zilizotengenezwa na Warumi, na uenezi wa lugha ya kimataifa (Kiyunani), ilichangia kasi ya uenezaji Injili. Lugha hiyo ndiyo iliyotumiwa na waandishi wote wa Agano Jipya ili vitabu vyao viwafaidishe watu wengi zaidi, ingawa baadhi yao hawakuijua vizuri.

Lugha asili ya Yesu na ya Mitume ilikuwa Kiaramu ambacho ni jamii ya Kiyahudi na ambacho polepole kilishika nafasi yake kati ya Wayahudi kuanzia karne VI K.K.

Mikoa ya Palestina wakati ule

[hariri | hariri chanzo]
Palestina katika karne ya 1 BK.

Hao wote walitokea mkoa wa Galilaya, uliokuwa chini ya Herode Antipa kuanzia mwaka 4 KK. Huko kulikuwa na mchanganyiko wa watu (Waisraeli na mataifa), kiasi kwamba huko Wayahudi wenyewe walifuata kwa urahisi desturi za Kiyunani hata wakadharauliwa na wenzao wa Kusini (Yerusalemu na mkoa wa Yudea).

Kati ya mikoa hiyo miwili ulienea mkoa wa Samaria ambao wakazi wake walijenga uadui mkubwa na Wayahudi baada ya uhamisho wa Babeli, walipokataliwa kuchangia ujenzi wa hekalu la pili la Yerusalemu. Samaria pamoja na Yudea ilikuwa chini ya liwali wa Roma kuanzia mwaka 6 BK.

Marejeo mengine

[hariri | hariri chanzo]

The Jewish Background of the New Testament Course (Dr. Eli Lizorkin-Eyzenberg) - http://eteacherbiblical.com/courses/jewish-background-new-testament?nav=left_sidebar Ilihifadhiwa 6 Februari 2015 kwenye Wayback Machine.

(1991), V.1, The Roots of the Problem and the Person ISBN 0-385-26425-9
(1994). V.2, Mentor, Message, and Miracles ISBN 0-385-46992-6
(2001). V.3, Companions and Competitors ISBN 0-385-46993-4
  • Neusner, Jacob Torah From our Sages: Pirke Avot ISBN 0-940646-05-6
  • Neusner, Jacob. Judaism When Christianity Began: A Survey of Belief and Practice. Louisville: Westminster John Knox, 2003. ISBN 0-664-22527-6
  • Orlinsky, H. M. ( 1971). "The Seer-Priest" in W.H. Allen The World History of the Jewish People, Vol.3: Judges pp. 269–279.
  • Pagels, Elaine The Gnostic Gospels 1989 ISBN 0-679-72453-2
  • Sanders, E.P. (1996). The Historical Figure of Jesus, Penguin ISBN 0-14-014499-4
  • Sanders, E.P. (1987). Jesus and Judaism, Fortress Press ISBN 0-8006-2061-5
  • Schwartz, Leo, ed. Great Ages and Ideas of the Jewish People. ISBN 0-394-60413-X
  • Vermes, Geza Jesus the Jew: A Historian's Reading of the Gospels. ISBN 0-8006-1443-7
  • Vermes, Geza, The Religion of Jesus the Jew. ISBN 0-8006-2797-0
  • Vermes, Geza, Jesus in his Jewish context. ISBN 0-8006-3623-6