Baraza hilo liliundwa na sheria ya bunge Na. 27 ya mwaka1967 kwa shabaha ya kukuza, kuimarisha na kuendeleza Kiswahili hasa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika marekebisho ya sheria hiyo yaliyofanyika mwaka 1983 kwa Sheria ya Bunge Na. 7, BAKITA imepewa uwezo wa kufuatilia na kusaidia ukuzaji wa Kiswahili katika nchi za nje pia.
Pamoja na Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA) cha Kenya na wawakilishi kutoka Uganda BAKITA imeunda Baraza la Kiswahili la Afrika Mashariki (BAKAMA).
Kukuza maendeleo ya matumizi ya lugha ya Kiswahili mahali pote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kushirikiana na vyombo vingine katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambavyo vinahusika na uendelezaji wa lugha ya Kiswahili na kuratibu kazi zao.
Kuhimiza matumizi ya Kiswahili katika shughuli za Serikali na kwa shughuli za umma.
Kuhimiza matumizi fasaha ya lugha ya Kiswahili na kuzuia upotoshaji wake.
Kushirikiana na mamlaka yanayohusika katika kuanzisha tafsiri sanifu ya istilahi za Kiswahili.
Kwa kushirikiana na vikundi vyovyote vya kimataifa, taasisi, au kundi la watu na watu binafsi, kufuatilia, kushauri na kuratibu shughuli zinazolenga kukuza Kiswahili.
Kuchunguza vitabu vya au maandishi yaliyoandikwa na kufasiriwa katika Kiswahili na kuhakikisha kwamba lugha iliyotumika ni sanifu na inakubaliwa na Baraza.