Dumuzi mdogo

Dumuzi mdogo
Dumuzi mdogo akitoboa punje za ngano
Dumuzi mdogo akitoboa punje za ngano
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Coleoptera (Wadudu wenye mabawa magumu)
Nusuoda: Polyphaga
Familia ya juu: Bostrichoidea
Familia: Bostrichidae
Nusufamilia: Dinoderinae
Jenasi: Rhyzopertha
Stephens, 1830
Spishi: R. dominica
(Fabricius, 1792)

Dumuzi mdogo (Rhyzopertha dominica) ni spishi ndogo ya mbawakawa ya familia Bostrichidae katika oda Coleoptera ambaye ni msumbufu wa hatari kwa sababu anaharibu nafaka zinazohifadhiwa maghalani. Spishi nyingine ya familia hii ni dumuzi mkubwa (Prostephanus truncatus) ambaye ni mkubwa kwa 50% zaidi ya dumuzi mdogo na ni msumbufu mbaya vilevile.

Dumuzi mdogo ana urefu wa mm 2-3. Mpevu ana umbo la mcheduara la kawaida la Bostrichidae. Rangi ni kahawianyekundu. Kichwa kimefichwa kutoka juu chini ya pronoto ambayo ina vijino kama mbuzi (ya nazi) kwenye mbele yake. Uso wa mwili una vijishimo. Vipapasio vina pingili 11 na vina kirungu chenye pingili tatu[1][2].

Mabuu ni weupe hadi rangi ya maziwa na wororo. Pande zao ni sambamba, yaani hazipunguzi. Miguu ni mifupi na kidonge cha kichwa ni kidogo kulinganisha na saizi ya mwili. Hatua za kwanza na pili zimenyoosha lakini hatua za tatu na nne zimepindika kama C[2].

Majike wa dumuzi mdogo hutaga mayai kati ya 200 hadi 500 katika maisha yao. Mayai hutagwa huru kwenye nafaka. Joto la chini kabisa ambamo dumuzi mdogo anaweza kumaliza maendeleo ni 20°C. Kwa halijoto hii ukuaji kutoka kwa yai hadi mpevu huchukua siku 90. Kiwango cha haraka zaidi cha ukuaji kinatokea kwa 34°C. Kwa halijoto hii mayai huchukua siku 2, mabuu siku 17 na mabundo siku 3 kukamilisha ukuaji. Dumuzi mdogo hawezi kukamilisha ukuaji wake juu ya 38°C. Wapevu huishi kwa muda wa miezi 4-8. Katika hali bora ya 34°C na unyevuanga wa nafaka wa 14% kuna ongezeko la mara 20 katika idadi ya dumuzi wadogo baada ya wiki 4. Wanaweza kufanikiwa kuvamia nafaka kwa kiwango cha unyevuanga wa 9%, lakini wana uzazi wa juu, ukuaji wa kasi na vifo vya chini kwenye nafaka ya kiwango cha juu cha unyevuanga.

Dumuzi mdogo anafikiriwa kutoka kwa kusini mwa Asia, lakini sasa anasambazwa katika maeneo ya kitropiki na maeneo ya wastani yenye joto kiasi kati ya 40º kaskazini na kusini. Katika Afrika ya Mashariki hadi sasa amerekodiwa tu katika Tanzania na Rwanda.

Mwenendo

[hariri | hariri chanzo]

Wapevu na mabuu wa dumuzi mdogo hula haswa mbegu za nafaka zilizohifadhiwa, pamoja na ngano, mahindi, mchele, oti, shayiri, mtama na mawele. Wanapatikana pia katika vyakula anuwai ikiwa ni pamoja na maharagwe, pilipili kavu, manjano, giligilani, tangawizi, chipsi za muhogo, biskuti na unga wa ngano. Kuna ripoti kadhaa za dumuzi mdogo akipatikana ndani au kushambulia mbao (Potter, 1935), kama ilivyo kawaida ya Bostrichidae wengine. Dumuzi mdogo imeripotiwa kuzalisha kizazi juu ya mbegu za miti na vichaka kadhaa (mwaloni, Celtis occidentalis (mti kama mmavimavi au mokalungo) na Symphoricarpos orbiculatus) (Wright et al., 1990).

  1. [1] Dumuzi mdogo kwenye EAFRINET
  2. 2.0 2.1 [2] Dumuzi mdogo kwenye CABI