Heinrich Albert Schnee (4 Februari 1871 - 23 Juni 1949) alikuwa mwanasheria kutoka nchini Ujerumani, mtumishi wa serikali na gavana wa mwisho wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.
Schnee alizaliwa huko Neuhaldensleben akiwa mtoto wa hakimu Hermann Schnee (1829-1901) na mkewe Emily. Alisoma shule ya sekondari huko Nordhausen halafu akasomea sheria huko Heidelberg, Kiel, na Berlin alipohitimu shahada ya uzamivu wa sheria mnamo mwaka 1893.
Mnamo 1897, aliaajiriwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Dola la Ujerumani. Mnamo 1898 alitumwa kwenda koloni la Kijerumani la Guinea Mpya alipokuwa mkuu wa wilaya na naibu gavana.
Mnamo 1900, alihamishwa kwenda Samoa ya Kijerumani alipopewa majukumu yaleyale.
Mnamo 1901 mjini New York alimwoa Ada Adeline Woodhill (1873-1969) aliyekuwa mwigizaji kutoka New Zealand.
Mwaka 1904 alirudi Berlin alipofanya kazi katika idara ya koloni ya Wizara ya Mambo ya Nje. Mnamo 1905 alihamishwa kwenda ubalozi wa Kijeurmani huko London, na kuanzia 1906 alirudi tena wizarani huko alipopanda ngazi hadi kuwa mkurugenzi wa kitengo cha kisiasa katika Ofisi ya Mambo ya Koloni. [1]
Mwaka 1912 Schnee aliteuliwa kuwa gavana wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani iliyokuwa koloni kubwa la Ujerumani. Mnamo Agosti 1914 Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ilianza pia katika Afrika. Akiwa gavana, Schnee alikuwa pia amiri jeshi katika eneo la koloni. Walakini tangu mwanzo wa vita hakukubaliana na kamanda wa Schutztruppe (jeshi la kikoloni), Paul von Lettow-Vorbeck, juu ya mikakati wa kujihami. Schnee alipenda kuepukana na mapigano na majirani Waingereza, lakini Lettow-Vorbeck alitaka kupigana nao kwa tumaini kwamba mapigano katika Afrika yangelazimisha Uingereza kutuma wanajeshi Afrika badala ya kuwatumia kule Ulaya; kwa njia hiyo alitumaini kwamba vita yake ingeweza kusaidia Ujerumani. Hatimaye von Lettow-Vorbeck alipuuza maagizo ya Schnee akaendelea kufuata mikakati yake na kudhibiti shughuli za kijeshi.
Hadi 1916 Schnee aliendelea kuwa na majukumu ya kiutawala; lakini kuanzia Januari 1916 Waingereza na Wabelgiji walishambulia kwa jeshi kubwa na hadi Agosti 1916 walithibiti tayari sehemu kubwa ya koloni. Schnee pamoja na maafisa wachache wa serikali yake walipaswa kuongozana na jeshi la Schutztruppe kwenye njia yake ya kujihami katika kusini ya Tanganyika hadi kukimbia hadi Msumbiji mwisho wa 1917, halafu kurudi Tanganyika 1918 hadi kupokea habari ya mwisho wa vita kwenye Novemba 1918 wakati walipokuwa waliingia Zambia.
Pamoja na mabaki ya jeshi Schnee alipelekwa Dar es Salaam na kutoka huko kwa meli hadi Ujerumani. [2]
Baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia Schnee aliingia katika siasa. Katika miaka iliyofuata Schnee alikuwa kati ya wanasiasa waliopinga masharti ya mkataba wa Versailles ambako Ujerumani ilipaswa kuachana na makoloni yote. Alikuwa mwenyekiti wa Umoja wa Wajerumani wa Ng'ambo (1926–1933), wa Shirika la Makoloni ya Ujerumani (Kolonialgesellschaft;1930–1936), na Shirika la Kijerumani kwa Maswala ya Shirikisho la Mataifa (1933–1945)
Kuanzia mwaka 1924 alikuwa mbunge wa chama cha liberali (DVP) alipojiuzulu mnamo 1932. Alikubali kuteuliwa mbunge tena na chama cha Nazi cha Adolf Hitler tangu mwaka 1933 akabaki na nafasi hiyo hadi 1945.
Schnee alifariki kutokana na ajali ya gari mnamo mwaka 1949 akiwa na umri wa miaka 78 akazikwa Berlin.