Sala ya kumiminiwa ni istilahi ya jaribio (kwa Kiingereza ni "Infused contemplation") kuhusu hali ya sala inayopatikana tu kwa neema maalumu ya Mungu hasa kwanzia hatua ya mwanga na zaidi katika hatua ya muungano ya maisha ya kiroho jinsi yanavyoelezwa na walimu kadhaa wa Kanisa Katoliki.
Tafakuri ni kazi ya akili inayotunga mawazo kadhaa ili kuchochea mapenzi kwa Mungu. Tukidumu katika njia hiyo, inakuja kuwa sala sahili ya mapendo ambamo hatua mbalimbali za tafakuri zinaelekea kuungana. Hivyo tunainuliwa polepole hadi kuzama katika mafumbo, yaani “kuzingatia kwa upendo, kwa usahili na kwa kudumu mambo ya Mungu”: hapo tunatazama kwa usahili sifa mojawapo ya Mwenyezi Mungu au mwanga wake unaorudishwa na kazi yake fulani. Kwa hiyo “sala inaitwa tafakuri kabla haijatengeneza asali ya ibada: baada ya hapo inakuwa ya kumiminiwa… Kama vile nyuki wanavyofonza katika maua, vivyo hivyo sisi tunatafakari ili kukusanya upendo wa Mungu, lakini kisha kuukusanya tunazama ndani ya Mungu na kuzingatia wema wake kutokana na utamu ambao upendo unatuonjesha humo”. Tofauti hiyo ya kwanza inasababisha ya pili: “Tafakuri inazingatia kinaganaga na kama sehemusehemu mambo yanayoweza kutugusa moyo; kumbe sala ya kumiminiwa ni mtazamo sahili sana unaokazania kinachopendwa… Hatusimami tena juu ya kipengele hiki wala hiki, bali tunafikia mtazamo wa jumla unaotulia ndani ya Mungu kwa mshangao na upendo, kama vile macho ya msanii yanavyotulia katika viumbe, au yale ya mtoto katika uso wa mama yake”.
Tofauti ya tatu inatokana na hizo mbili: tafakuri inafanyika kwa uchovu, kumbe “sala ya kumiminiwa inafanyika kwa raha, maana inadai kwanza tumpate Mungu na upendo wake mtakatifu”. Hata hivyo kuna saa za giza ambamo roho inasikitikia kumkosa kwa jinsi inavyomtamani, na ambamo katika jaribu inajiunga na matakwa yake.
“Kwa kuwa sala ya kumiminiwa ndiyo lengo na shabaha ya vitendo vyote vya Kiroho, inavijumlisha vyote”; lakini “namna hiyo ya kujikusanya hatuisababishi kwa uamuzi wetu, kwa maana hatuwezi kuwa nayo tunapotaka; haitegemei juhudi zetu ila Mungu anaitokeza ndani mwetu kwa neema yake takatifu anapotaka mwenyewe”.
Tendo lolote la kuzama kwa akili ni la juu kuliko mifuatano ya mawazo, ni mtazamo sahili wa ukweli. Lile linalozungumziwa na watakatifu linatokana na upendo na kuhitaji uvuvio maalumu wa Roho Mtakatifu, ambao vipaji vyake vinatuandaa kuupokea mara kama vile tanga za boti zinavyopokea msukumo wa upepo. Ndiyo sababu sala hiyo inastahili kuitwa ya kumiminiwa, ingawa mara nyingi inaandaliwa na somo, tafakuri na maombi. Kwa njia hizo mtu anajiandaa kupokea uvuvio wa Roho Mtakatifu, ambao pengine utakuwa na nguvu ya kutosha isihitaji tafakuri, kama vile upepo mzuri wenye nguvu za kusukuma boti unavyofanya kazi ya wapigakasia isihitajike tena.
Ili kutuonjesha mafumbo ya imani uvuvio huo maalumu unatumia mvuto wa mambo ya Kimungu unaotegemea upendo. “Ndio ukamilifu mkuu wa sala ya kumiminiwa, kwamba ukweli wa Kimungu usionekane tu, bali upendwe pia”. Uvuvio huo unasababisha tendo la kumiminiwa la upendo na la imani hai yenye kupenya na kuonja linalotuonyesha jinsi mafumbo yaliyofunuliwa yanavyoitikia vizuri ajabu matamanio yetu ya juu na ya dhati zaidi ingawa bado yana giza kwetu. Matendo hayo ni ya kumiminiwa si kwa sababu tu yanatokana na maadili ya kumiminiwa, bali kwa sababu yanahitaji uvuvio maalumu wa Roho Mtakatifu, kwa kuwa hatuwezi kuyafikia kwa msaada wa neema za kawaida. Kwa mfano, tukisoma Injili, ghafla neno tulilokwishalisoma mara elfu linatuangaza na kutuvutia; au mhubiri akijitambua hawezi kusema inavyofaa juu ya mateso ya Yesu siku ya Ijumaa Kuu, kisha kuanza anapokea uvuvio unaohuisha akili yake, utashi wake na hisi zake kwa faida ya wasikilizaji.
Pengine mtazamo huo unainuka wima kwa Mungu, k.mf. kutoka tendo fulani au mfano wa Injili hadi kushangaa huruma ya Mungu. Pengine una mwendo wa pia, k.mf. kutoka mafumbo ya wokovu hadi wazo hai la dhati la uzima wa milele. Pengine tena ni mtazamo wa mzunguko wa wema usio na mipaka wa Mungu unaong’aa juu ya yote; ni mtazamo sahili uliojaa upendo, unaofanana na mruko wa tai juu hewani, anapokazia macho jua na uenezi wa mwanga wake.
Mpito kati ya sala ya kujipatia na ile ya kumiminiwa unaeleweka zaidi tukifuata maandishi ya Teresa wa Yesu kuhusu aina ya mwisho ya sala za kujipatia na ile ya kwanza ya sala za kumiminiwa.
Tusome alivyofafanua aina bora ya sala za kujipatia: “Inaitwa sala ya kujikusanya kwa sababu hapo roho inakusanya vipawa vyake vyote na kujifungia ndani pamoja na Mungu wake. Kwa njia hiyo Mwalimu wake wa Kimungu ataifundisha na kuijalia sala ya utulivu mapema kuliko kwa njia nyingine yoyote. Roho ikiwa imejificha ndani mwake inaweza kufikiria mateso, kujichorea Mwana wa Mungu na kumtolea Baba isihitaji kujichosha ikamtafute huko Kalivari, au bustanini pa mizeituni au mnarani. Watakaoweza kujifungia hivyo ndani ya mbingu ndogo za roho zao anamokaa Muumba wao… watakaozoea kuzuia macho yao, kusali mahali pasipo kitu kinachoweza kutawanya hisi za nje, wawe na hakika ya kufuata njia bora na ya kuweza kunywea chemchemi ya uhai. Hakika watasonga mbele sana kwa muda mfupi… Huko kujikusanya kama ni kwenyewe kunatambulikana kwa urahisi kwa njia ya tokeo lake fulani. Sijui namna ya kujieleza, lakini mwenye mang’amuzi hayo atanielewa vizuri. Tungesema kuwa roho, ikiona malimwengu ni upuuzi tu, inainuka ghafla na kuyaacha. Au kwamba mtu, akitaka kujihami na adui yake, anaingia ndani ya ngome. Hisi zinajikusanya mbali na vitu vya nje na kuvisogeza mbali kwa dharau sana, hata mtu bila kujitambua anakuja kufumba macho asivione tena na hivyo afanye mtazamo wa roho upenye zaidi. Kweli wanaofuata njia hiyo wanafumba macho karibu mfululizo wanaposali. Zoea hilo ni zuri ajabu pande zote… Tukidumu kujilazimisha muda fulani tutaona wazi faida itakayopatikana. Mara tutakapoanza kusali tutaona nyuki kuja kwenye mzinga na kuingia watengeneze asali. Hilo halina juhudi yoyote kwa sababu roho kama malipo ya yale iliyoyafanya kwanza imestahili kutawala hivyo hisi kwa njia ya utashi. Ikitoa tu ishara ya kutaka kujikusanya, hisi zinaitii na kujikusanya ndani yake… Atakayetaka kujipatia zoea hilo, ambalo narudia kusema limo ndani ya uwezo wetu, asichoke kulifanyia kazi… Mkijitahidi kweli mtafaulu kwa mwaka mmoja, na pengine kwa miezi sita. Je, si kidogo sana kwa faida kubwa namna hii? Tena kwa kufanya hivyo mnaweka msingi imara, na Bwana akipenda kuwainua kwenye makuu, atawakuta mko tayari, kwa kuwa mnabaki karibu naye zaidi”. Ndivyo sala ya kujipatia inavyotuandaa kwa ile ya kumiminiwa.
Akafafanua hivi sala ya kwanza ya kumiminiwa: “Naona hiyo ni namna ya kukusanyika ipitayo maumbile. Kiini chake si kwenda gizani wala kufumba macho… Ingawa pasipo kutaka tunafumba macho na kutamani upweke. Inavyoonekana ndipo jumba la sala nililolizungumzia linapojengwa pasipo kazi ya ufundi… Msidhani huko kukusanyika kunapatikana kwa kazi ya akili, kwa kujitahidi kumfikiria Mungu ndani mwetu, au kwa kazi ya ubunifu, kwa kujichorea alivyo… Si namna hiyo ya kutenda ambayo kila mmoja anaiweza, bila shaka daima kwa msaada wa Mungu. Ninayoongelea ni tofauti. Pengine, hata kabla hatujaanza kumfikiria Mungu… tunang’amua wazi kabisa utamu wa kukusanyika… Hilo halitegemei utashi wetu: linatokea tu Mungu anapotaka kutujalia neema hiyo. Nadhani Mungu anachagua kuwajalia watu walioachana na malimwengu… Naamini pia tukimuachia Mungu uhuru wake wa kutenda, hatazuia ukarimu wake kwa wale anaowaita wazi kupanda juu zaidi”. Asipojalia bado neema hiyo, haiwezekani “kufunga akili kwa faida kubwa kuliko hasara”.
Hayo yote yanalingana na mafundisho ya Yohane wa Msalaba: “Katika sala ya kumiminiwa Mungu analisha na kuimarisha roho pasipo hiyo kuchangia kwa kazi au mawazo yoyote ya makusudi”. Kwa hakika kazi ya maadili inatakiwa kuendelea, hata kwa matendo ya kishujaa, lakini sala inazidi kuwa sahili, na mtu anapaswa hasa kupokea kwa mikono miwili uvuvio wa Roho Mtakatifu.
“Huko kutazama gizani ndiyo teolojia ya mafumbo ambayo walimu wanaiita hekima ya siri, na ambayo kadiri ya mafundisho ya Mt. Thoma inashirikishwa kwa njia ya upendo kumiminwa rohoni”. Huo utekelezaji bora wa maadili ya Kimungu na ya vipaji vinavyoendana nayo ukidumu muda fulani unaitwa hali ya sala. Ni hali ya kumiminiwa kwa sababu hatuwezi kuisababisha ila kujiandaa tuipokee, kwa kudumu katika sala, kubeba kila siku msalaba wetu na kuwa wasikivu kwa Roho Mtakatifu. Hapo imani hai inakuwa imani ya kupenya na mara nyingi imani ya kuonja, iweze kuishi kwa dhati mafumbo yaliyofunuliwa.
Mafundisho ya mapokeo tuliyoyaeleza yamethibitishwa na Kanisa Katoliki kwa kulaani maneno kadhaa ya kizushi ya Mikaeli Molinos na Watulivu kwa jumla.
Kadiri yao mtu anapaswa kunyamazisha vipawa vyake, kwa sababu kutaka kutenda ni chukizo kwa Mungu anayetaka kutenda peke yake ndani mwetu. Utendaji ni adui wa neema, nadhiri ya kutenda jambo ni kizuio cha ukamilifu, roho isipotenda inajiangamiza na kuirudia asili yake: hapo Mungu anatawala na kuishi ndani yake. Ndiyo njia ya Kiroho ambapo mtu hatendi kwa kumjua wala kumpenda Mungu, tena hafikirii uzima wa milele wala adhabu za motoni. Mtu hatakiwi kutamani ajue kama anampendeza Mungu au la, wala kufikiria matendo na makosa yake ili kujirekebisha; hatakiwi kutamani ukamilifu na wokovu wa milele, wala kumuomba Mungu neno maalumu; hahitaji kupambana na vishawishi, ila asivijali.
Kwa kufundisha hayo, Molinos alifuta kwa mkupuo mmoja juhudi zote na utekelezaji wa maadili ambayo ndiyo maandalizi halisi ya sala ya kumiminiwa na ya muungano na Mungu. Hivyo alipotosha maisha yote ya Kiroho.
1) Kuna njia moja tu, yaani sala ya kumiminiwa, ambayo tunaweza kujipatia kwa neema ya kawaida tukikoma kutenda lolote. Basi tuiingie mapema iwezekanavyo. 2) Tendo la sala ya kumiminiwa linaweza kudumu miaka, hata maisha yote, usingizini pia, bila kuchochewa. 3) Kwa kuwa sala ya kumiminiwa ni ya kudumu, inaturuhusu tuache kutekeleza maadili (k.mf. imani, tumaini, ibada na toba); hayo yanawafaa wanaoanza tu. 4) Kumfikiria Yesu na mafumbo yake ni kasoro; kuzama katika umungu tu ni kwa lazima, tena kunatosha. Anayetumia picha au mawazo hamuabudu Mungu katika Roho na ukweli. 5) Katika hali ya sala ya kumiminiwa tunatakiwa kutojali lolote, hata utakatifu na wokovu wetu, bali tupoteze tumaini ili upendo usiwe wa kujitafutia faida. 6) Tusisumbuke kupinga vishawishi: mawazo na matendo machafu ni majaribu yaliyowapata watakatifu pia; hayana lawama kwa sababu ni kazi ya shetani, hivyo hatutakiwi kuyaungama. Ndivyo tunavyofikia kujidharau na kuungana kwa ndani na Mungu.
Mafundisho ya Kikatoliki yanayopinga uzushi huo ni kama ifuatavyo: 1) Kuna hali ya kutendewa ambapo Mungu mwenyewe anatenda ndani mwetu; lakini kwa kawaida tunaifikia baada tu ya kutekeleza muda mrefu maadili na tafakuri. 2) Kwa kawaida tendo la sala ya kumiminiwa linadumu muda mfupi, ingawa hali ya roho inayotokana nalo inaweza ikadumu siku kadhaa. 3) Sala ya kumiminiwa, inayoendana na tendo la kumpenda Mungu, inatimiliza maadili yote, lakini haituruhusu tuache kuyatekeleza nje ya sala. 4) Jambo kuu ambalo tuzame ndani yake ni Mungu mwenyewe, lakini Yesu ndiye la pili; nje ya tendo la sala ya kumiminiwa tusiache kumfikiria mshenga huyo wa lazima wala kumuendea Mungu tusimpitie. 5) Kujiachilia kitakatifu ni njia kamili, lakini bila kufikia hatua ya kutojali wokovu wa milele; kinyume chake tunapaswa kuutamani, kuutumaini na kuuomba. 6) Katika majaribu ya Kiroho ubunifu na hisi vinaweza vikavurugika, huku sehemu ya juu ya roho ikifurahia amani; lakini utashi unapaswa daima kupinga vishawishi (walau kwa kutovizingatia au kwa kupoteza lengo) usije ukavikubali.
Ngazi za sala ya kumiminiwa ni zile za ustawi wa mfululizo wa imani, upendo na vipaji vya Roho Mtakatifu. Kwa namna fulani ustawi huo wa muungano na Mungu unadhihirika kwa hali hiyo kuzidi kuenea katika vipawa mbalimbali, ambavyo polepole vinavutwa na Mungu hata ikakoma mitawanyiko ya mawazo inayotokana na ubunifu usiotulia wala kuratibika. Zaidi ya hayo, maadili kwa kawaida yanastawi kadiri sala inavyoendelea.
Teresa wa Yesu ameonyesha hayo akifananisha ngazi za sala na namna nne za kumwagilia bustani. Ya kwanza ni kutoa maji kisimani kwa nguvu ya mikono tu; ni mfano wa tafakuri yenye mifuatano ya mawazo inayochangia ustawi wa maadili. Ya pili ni kupandisha maji kwa chombo cha kurahisishia uvutaji wa kamba; ni mfano wa sala ya utulivu inayoandaliwa na kazi yetu: hapo maua ya maadili yanakaribia kuonekana. Ya tatu ni kupitisha bustanini maji ya mto; katika sala hiyo maadili yanapata nguvu nyingi kuliko awali na maua yake yanachanua. Ya nne ni mvua, mfano wa sala ya muungano ambayo Mungu anamjalia mtu pasipo huyo kuchoka: “katika sala hiyo anachota mema mengi zaidi sana na unyenyekevu wake unakua. Ndipo vinapotokea ahadi na maazimio ya kishujaa, hamu motomoto, chuki kwa ulimwengu, mtazamo wazi wa ubatili”.
Teresa wa Yesu alieleza maendeleo ya sala ya kumiminiwa kwa kusisitiza uenezi wa utawala wa Mungu juu ya vipawa vya roho, kimoja baada ya kingine, lakini alijua kuwa tukio la ubunifu na hisi kusimamishwa si la msingi wala la lazima, kwa sababu katika hali kamili kupita zote, yaani muungano unaotugeuza, mtu kwa kawaida hatoki tena nje ya nafsi yake. Hivyo uenezi si mamoja na udhati, ila ni dalili rahisi kutambulikana na kuelezwa; inafaa mradi iendane na nyingine ya ndani zaidi, yaani matakaso ya Kimungu yanayoonyesha maendeleo makubwa katika kumjua na kumpenda Mungu na katika maadili mengine.
Yohane wa Msalaba alisema hayohayo, akionyesha katika usiku wa hisi mwanzo wa sala ya kumiminiwa pamoja na hamu kubwa ya Mungu: ni utulivu mkavu unaoandaa ule mtamu ulioelezwa na Teresa katika makao ya nne.
Basi sala ya kumiminiwa inaanza na takaso la Kimungu la hisi, ambalo ni uongofu wa pili katika utulivu mkavu, inaendelea na nderemo za hatua ya mwanga, inapenya zaidi wakati wa usiku wa roho katika majaribu makali dhidi ya maadili ya Kimungu, ambapo maadili hayo na unyenyekevu yanatakata na kuwa ya kishujaa kweli, hata mtu anakuwa tayari kwa muungano unaotugeuza ulio kilele cha sala ya kumiminiwa.
Katika utulivu mtamu, unaoitwa pia sala ya nderemo za Kimungu (aina ya pili ya umwagiliaji wa roho kadiri ya Teresa wa Yesu), “utashi tu umetawaliwa” na nuru ya uhai inayodhihirisha uwemo mtamu wa Mungu ndani mwetu na wema wake. Hapo kipaji cha ibada kilichomo ndani ya utashi kinauelekeza kumpenda kitoto. Ni kama mtoto mchanga anayeonja maziwa anayopewa, au vizuri zaidi ni kama bubujiko la maji hai ambayo “yanatokana na chemchemi yenyewe, yaani Mungu… yanatiririka kutoka kina cha undani wetu kwa amani, utulivu na utamu mkuu… Maji hayo ya mbinguni yakianza kububujika kutoka chemchemi yake… mara ni kana kwamba undani wetu wote unatanuka na kupanuka. Hapo yanatujia mema ya Kiroho yasiyosemekana, na mhusika hawezi kuelewa anayoyapata wakati huo”.
Lakini katika hali hiyo akili, kumbukumbu na ubunifu havijatawaliwa na kazi ya Mungu: pengine vinasaidia na kutumikia utashi, pengine vinauvuruga tu. Hapo utashi usivijali kuliko “jinsi ya kumshughulikia kichaa”. Ingawa mara nyingi huo utulivu mtamu unakatizwa na ukavu na majaribu ya usiku wa hisi, na vishawishi vinavyodai vipingwe kwa nguvu, matokeo yake ni uadilifu mkubwa zaidi, hasa upendo mkubwa zaidi kwa Mungu na amani isiyovurugika, walau katika sehemu ya juu ya roho.
Sala ya utulivu ina hatua tatu: 1) mtu kujikuta anakusanyika, hali ambayo ni neema ya pekee ya kufyonza matakwa ya Mungu kwa utamu na upendo; 2) utulivu wenyewe ambapo utashi unapatwa na Mungu ukiwa unabaki kimya au unasali kama umelewa Kiroho; 3) usingizi wa vipawa ambapo, utashi ukiendelea kutawaliwa na Mungu, akili inaacha kufuata mawazo na inakuja kupatwa na Mungu vilevile, ingawa kumbukumbu na ubunifu vinaendelea kutikisika.
La kufanya katika hatua hizo ni kujiachilia kwa unyenyekevu mikononi mwa Mungu. Mtu asijaribu kuingia hali hiyo, inayoweza kutokana tu na neema maalumu ya Roho Mtakatifu ambaye mara anatuelekeza kunyamaza kwa upendo, mara kububujika mapenzi kama maji ya chemchemi. Ikiwa akili na ubunifu vinatawanyika, hakuna haja ya kuhangaika au kuvifuatia; utashi uendelee kufurahia fadhili uliyojaliwa, kama nyuki katika chumba cha mzinga.
Mtu akiwa mwaminifu – si tu katika kutimiza kwa makini wajibu wowote wa kila siku, bali pia katika kusikiliza minong’ono ya Roho Mtakatifu anayezidi kudai kadiri anavyofadhili – basi kwa kawaida anainuliwa hadi “muungano sahili”. Hapo kazi ya Mungu inakuwa na nguvu za kutosha ivute vipawa vya roho ambayo kazi yake yote inakuja kumuelekea yeye badala ya kupotea nje. Si utashi tu unatawaliwa naye (kama katika sala ya utulivu), bali pia akili na kumbukumbu, hata mtu ni kama ana hakika ya uwemo wa Mungu. Ubunifu hautikisiki tena, bali unatulia; pengine ni kama umesinzia ili kuacha akili na utashi viungane na Mungu. Hapo neema ya pekee ya Roho Mtakatifu ni kama maji yanayotiririka bustanini toka mtoni, kwa kutumia mfano wa Teresa wa Yesu.
Inatokea pia kwamba utendaji wote wa roho uende upande wake wa juu, hata kuna kusimamishwa kwa muda kwa hisi za nje, yaani mwanzo wa kutoka nje ya nafsi kama si kutoka kwenyewe. Ikiwa pengine mtaalamu aliyezamia somo lake hasikii anachoambiwa, zaidi tena itamtokea mtu aliyevutiwa na Mungu. Hapo anapokea maji hai ambayo yanaburudisha na kutakasa kama mvua toka mbinguni, kwa kutumia mfano mwingine wa Teresa wa Yesu, aliyesema, “Mungu hamuachii kutoa mchango mwingine isipokuwa ule wa utashi uliotawaliwa kabisa… Jinsi ilivyo nzuri hali inayompata kisha kuzama katika ukuu wa Mungu na kuungana kabisa naye, ingawa kwa muda mfupi, kwa sababu nionavyo mimi muungano huo haufikii kamwe nusu saa!”
Teresa anasema pia hiyo sala ya muungano mara nyingi si kamili, yaani ubunifu na kumbukumbu havisimamishwi, bali vinavipiga vita akili na utashi: “Kwa muungano tunaouzungumzia hapa, je, ni lazima vipawa hivyo visimamishwe? Hapana. Bwana anaweza kuwatajirisha watu kwa njia mbalimbali na kuwafikishia makao hayo bila kuwapitisha njia ya mkato niliyoielekeza”, yaani utamu wa kutokuwa na mitawanyiko ya mawazo, wa kutochoka na wa kusikia nderemo kwa wingi.
Matokeo ya sala ya muungano ni mtu kubadilika kama mdudu anapokuwa kipepeo. Anasikia majuto makubwa kwa makosa yake; anapata ari motomoto ya kumtumikia Mungu na kumtangaza ili apendwe; anaumia kuona wakosefu wakipotea;anahisi mateso ya Bwana yalivyokuwa. Hapo anaanza kutimiza maadili kishujaa, hasa kutii kikamilifu matakwa ya Mungu na kumpenda jirani. Pengine wafiadini walijaliwa sala hiyo katikati ya mateso yao.
Sala ya utulivu mtamu na ya muungano sahili zinapatikana kati ya matakaso ya Kimungu ya hisi na roho. Maana kwa kawaida kuna kipindi cha amani katika ya hayo mawili, yaani usiku wa hisi (mwanzo wa makao ya nne) na usiku wa roho (makao ya sita) unaoingiza katika muungano mkavu na muungano wa kutoka nje ya nafsi hadi kufikia muungano unaotugeuza.
Waliyoyasema walimu wa Kiroho kuhusu sala ya kumiminiwa si ya juu mno kwa mtu anayefuata njia ya unyenyekevu na kujikana, akizidi kuelewa kwamba Mungu “amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; na wanyonge amewakweza” (Lk 1:52). Si ya juu mno kwa mtu anayeamini kwamba katika ubatizo amepokea mbegu ya uzima wa milele, na anayetambua haja ya kuzidi kusadiki thamani isiyo na mipaka ya ekaristi. Muhimu ni kupokea toka kwa Mungu yale yote anayotaka kutupatia kwa huruma yake isiyo na mipaka ili kutuvuta kwake na kutushirikisha milele uzima wake wa ndani na heri yake isiyo na mwisho.
Wote wanakubali kwamba mtu yeyote anaweza akatazama ukweli kwa usahili, pasipo mifuatano ya mawazo, k.mf. kuuona katika viumbe wenye mchanganyiko na mabadiliko uwepo wa uhai wenyewe, ulio sahili tu, usiobadilika, ulio asili na lengo la vyote. Thibitisho zote za falsafa kuhusu uwepo wa Mungu zinalenga kilele hicho, ambacho akili inaweza kukifikia kwa nguvu zake na msaada wa kawaida wa neema.
Lakini kuhusu mtazamo sahili wa Kikristo, unaotegemea kupokea kwa imani ufunuo wa Mungu, walimu wa Kiroho wana maana gani wanapoutofautisha na tafakuri ya Kikristo ambayo pia inahusu kweli za imani na yanayotokana nazo? Jibu ni kwamba, “sala hasa ni ujuzi wenye upendo kumhusu Mungu tunaomiminiwa” (Yohane wa Msalaba), ujuzi ambao haututeki daima, bali pengine unaendana na mitawanyiko ya mawazo na ukavu wa matakaso ya Kimungu. Ni tofauti na tafakuri inayotegemea mifuatano ya mawazo hata inapozidi kuwa sahili.
Kisha kutafakari tunaweza tukafikia kumjua Mungu na kazi zake kwa usahili na upendo kama tunda la juhudi zetu zikisaidiwa na neema. Mtazamo huohuo wanaweza kuwa nao: mwanateolojia akijumlisha aliyoyajua kwa utafiti wake; au mhubiri anayeona hotuba yake yote katika wazo kuu; au msikilizaji wake anayeshangaa umoja wa maneno yake na kufurahia mwanga wa ukweli. Huo unatokana na imani ikiendana na upendo, tena na athari wazi kidogo za vipaji vya akili, hekima na elimu; lakini usingekuwepo bila kazi ya kupanga vizuri mawazo ili kuonyesha yanavyolingana. Mkristo anayefikiria ukweli fulani wa imani anaweza akafikia tafakuri sahili ya kimapenzi, aina ya sala ya kimapenzi au sala ya kujikusanya kwa makusudi, ambapo asimame muda mfupi kutazama kwa usahili na mshangao wema wa Mungu au maongozi yake au stahili za Mwokozi; halafu akarudia mifuatano ya mawazo na mapenzi.
Kumbe toka tafakuri tunaweza tukavukia “hali ambayo Mungu anajishirikisha kwa mtu asiyetenda lolote, kama mwanga unavyomfikia mwenye macho wazi” (Yohane wa Msalaba). Sala hiyo ya kumiminiwa si tunda la utendaji wa mtu kwa msaada wa neema, bali la uvuvio maalumu wa Roho Mtakatifu. Kwa mfano, katika hotuba ya kukinaisha tu, linatajwa neno la Bwana linalokuja kumgusa na kumteka mtu fulani: hilo ni tendo la wazi la sala ya kumiminiwa, kwa sababu yeye hawezi kulisababisha kama anavyoweza kutekeleza imani namna ya kawaida. Tendo hilo ni la pekee, linatokana na imani yenye kupenya na pengine hata kuonja, ambamo kiongozi stadi anatambua mapema athari za vipaji vya akili na hekima. Ingawa hatuwezi kulisababisha, tunaweza kujiandaa kupokea uvuvio wa Kimungu unaolisababisha, na tunaweza kuufuata. Hivyo tendo la upendo wa kumiminiwa ni la hiari na lenye kustahili kutokana na usikivu kwa Roho Mtakatifu ulionalo.
Hiyo sala ya kumiminiwa inaanza mtu anapojikuta akikusanyika katika usiku wa hisi. Hali hiyo ikidumu na kujirudiarudia, mtu ameshaingia maisha ya mafumbo.
Sala ya kumiminiwa haitokani tu na maadili ya kumiminiwa, bali ni tendo la kumiminiwa la ujuzi linaloendana na upendo wa kumiminiwa, tusiloweza kulitenda wenyewe kwa msaada wa neema ya kawaida. Kwa baadhi unatawala upendo, kwa baadhi mwanga. “Ujuzi huo wenye giza unaitwa wa siri, na Mt. Thoma alisema unashirikishwa na kumiminwa na upendo rohoni. Unashirikishwa kwa siri, pasipo mchango wa utendaji wa kimaumbile wa akili wala wa vipawa vingine. Kwa kuwa hivyo haviwezi kuupata, ila Roho Mtakatifu ndiye anayeumimina rohoni kwa fadhili, ndiyo sababu ni wa siri kweli” (Yohane wa Msalaba). Kwa uvuvio huo toka juu imani hai inazidi kupenya na kuonja.
Basi, tofauti kati ya sala ya kumiminiwa na tafakuri yoyote si ya ngazi tu bali ya mfumo. Kwa kuwa tafakuri inategemea uwezo wetu, inatokana na utendaji wetu ukisaidiwa na neema ya kawaida; athari ya vipaji vya Roho Mtakatifu ikiwepo, siyo inayoisababisha, bali inaisaidia tu, kama kazi ya wapigakasia inavyosaidiwa na upepo wa kuwaburudisha. Kinyume chake sala ya kumiminiwa haitegemei uwezo wetu, bali uvuvio maalumu wa Roho Mtakatifu ambao si neema kubwa ya msaada, bali unaendesha kwa kufuata kanuni ya juu. Ndivyo vilivyo tofauti maadili ya kumiminiwa na vipaji vya Roho Mtakatifu. Maadili ya kumiminiwa ni asili ya matendo tunayoweza kuyasababisha, kumbe vipaji vinatuandaa kupokea kwa mikono miwili msukumo wa Roho Mtakatifu kwa matendo ambayo namna yake ipitayo maumbile na itokanayo na kanuni ya juu inazidi utendaji wetu unaosaidiwa na neema ya kawaida.
Katika maisha ya juhudi, kabla ya takaso la Kimungu la hisi lililo mwanzo wa sala ya kumiminiwa, vipaji vya Roho Mtakatifu vinaathiri kidogo tu, na mara nyingi ni kama vimefungwa na ambatano fulani na dhambi nyepesi. Baadaye, katika maisha ya mafumbo vipaji vya akili na hekima vinakuja kuonekana: kwa baadhi ya watu hasa kwa namna ya kutazama ukweli, kwa baadhi kwa namna inayoelekea zaidi utendaji.
Matendo ya sala ya kumiminiwa hayana mifuatano ya mawazo hata kidogo, bali ni mtazamo sahili; pengine ni matulivu kiasi kwamba mhusika hayaoni, tofauti na yale anayoyakusudia. Kwa hiyo Antoni abati alisema, “sala si kamili mkaapweke akijitambua anasali”. Ndio “ujinga wenye ujuzi” uliozungumzwa na walimu wa Kiroho. Matendo manyofu ya sala ya kumiminiwa hayana uvivu wowote wa hatari, bali ujuzi wa dhati wa ukweli wa Mungu. Ikiwa mtu, kisha kusali hivyo, anajikuta mnyenyekevu, mtulivu, amebandukana na yote, ana ari kwa utekelezaji wa maadili, maana yake hakupoteza muda wake.
Mambo muhimu yafuatayo yanatokana na yale tuliyoyasema:
1) Sala hiyo, katika ngazi zake, haileti furaha daima: kwa kawaida inaanza katika ukavu wa hisi na inaweza kudumu katika ukavu mkubwa wa roho. Vilevile si lazima iondoe uwezo wa kupanga mawazo: ni ya juu kuliko mifuatano ya mawazo, lakini kwa sababu hiyohiyo inaweza kuiongoza kutoka juu, k.mf. wakati wa kuhubiri au kuandika.
2) Kuzama katika mafumbo kunaleta pengine utambuzi wa uwepo wa Mungu (ujuzi unakaribia kuwa mang’amuzi kutokana na kipaji cha hekima), pengine kiu kubwa ya Mungu pamoja na uchungu mwingi kwa kutoweza kumfurahia na hisi kali ya kuwa mbali naye kimaadili na Kiroho (hasa katika usiku wa roho, ambapo upenyaji wa kipaji cha akili unajitokeza kuliko mwonjo wa kipaji cha hekima). Katika hali hiyo ya mwisho ujuzi wa kumiminiwa na upendo wa kumiminiwa vinasababisha uchungu mkali kwa kuona Mungu hapendwi inavyotakiwa. Uchungu huo na kiu hiyo haviwezi kuwepo pasipo athari ya dhati ya neema: hivyo ni uwemo mchungu wa Mungu.
3) Sala ya kumiminiwa haidai mawazo ya kumiminiwa kama yale ya malaika, ila mwanga wa kumiminiwa, yaani mwanga maalumu wa vipaji ambavyo ni tofauti na karama zinazotolewa hasa kwa faida ya wengine (k.mf. kutabiri au kupambanua roho).
4) Yenyewe si kumhisi moja kwa moja Mungu alivyo, lililo jambo maalumu la heri ya milele. Kwa athari kubwa ya kipaji che hekima, uwemo wa Mungu unajulikana pasipo mifuatano ya mawazo, kwa njia ya matokeo yake, hasa upendo wa kitoto anaotuvutia kwake na utamu wa upendo anaouonjesha mara kadhaa.
5) Tangu hapo maisha ya Kiroho yanatawaliwa na namna ipitayo maumbile ya vipaji vya Roho Mtakatifu, hasa kile cha hekima kinachoviangaza vingine; utawala huo umekuwa unajirudiarudia na ni wazi kwa kiongozi stadi. Hata hivyo, katika usiku wa hisi kipaji cha elimu ndicho kinachotawala kikionyesha ubatili wa malimwengu; halafu katika usiku wa roho tunakuta hasa kipaji cha akili kikipenya mafumbo, pasipo kuonja ladha yake kwa kipaji cha hekima, kinachojitokeza katika ustawi wake wote wakati wa muungano unaotugeuza tu. Hatutakiwi kuichanganya hali ya kuzama katika mafumbo kwa jumla na vipindi vyake vyenye faraja, wala kuichanganya na utimilifu wake, kwa kuwa mara nyingi ina namna ya utulivu mkavu.
Kuna watu wanaodhani maelezo haya kuhusu sala ya kumiminiwa hayatoshi kwa kuwa, eti! Hayaonyeshi vya kutosha yaliyo mapya katika sala hiyo, hata tofauti yake na sala ya kujipatia inaonekana kuwa ya kiwango tu, kwa sababu hiyo ya pili nayo inachangiwa na vipaji vya Roho Mtakatifu ingawa si wazi. Basi, tuzingatie zaidi.
Upya wa sala ya kumiminiwa unaonekana wazi mtu akivuka mara toka tafakuri sahili hadi utulivu mtamu ambapo utashi unatawaliwa na mwanga wa ndani (unaouonyesha wema wa Mungu uliomo ndani mwake kama chemchemi ya maji hai) ingawa akili na ubunifu vinaleta vurugu. Upya huo ungeonekana wazi zaidi kama akili pia ingetawaliwa, na ubunifu na kumbukumbu vingetulia inavyotokea katika sala ya muungano.
Lakini mara nyingi mtu havuki hivyo, bali mwanzo wa sala ya kumiminiwa unaendana na ukavu wa hisi wa muda mrefu, hata ukaitwa utulivu mkavu. Hapo upya huo hauonekani wazi, kwa kuwa athari za uvuvio maalumu wa Roho Mtakatifu zinaanza tu kujitokeza. Wenye juhudi wanaweza wakamiminiwa sala wasitambue, kwa sababu hali hiyo inakuwepo hata katika giza nene. Basi, upya huo hauonekani kila mara, tena hata ukiwa wazi kiasi, si sawa katika utulivu mkavu na katika ule mtamu.
Mtu akivuka hatua kwa hatua, uvuvio maalumu unaopokewa na vipaji vya Roho Mtakatifu unaeleza vya kutosha upya wake, mradi tuone vizuri tofauti iliyopo kati ya namna ya kibinadamu ya maadili (hata yale ya Kimungu) na namna ipitayo maumbile ya vipaji vya Roho Mtakatifu, ambavyo matendo yake yanaratibiwa moja kwa moja na uvuvio wake maalumu. Uvuvio huo ni neema inayotenda ambayo inatufanya tutende kwa hiari pasipo kuamua kwa mifuatano ya mawazo; hivyo ni ya juu kuliko neema za kawaida ambazo zinasaidia kutenda kwa kuamua kwa mifuatano ya mawazo.
Ndiyo tofauti iliyopo kati ya vipaji na maadili yote: uvuvio maalumu wa Roho Mtakatifu ni kanuni ya Kimungu inayosababisha utendaji upitao ubinadamu. Kwa mfano, nikiona imefika saa ya kusali naenda mwenyewe (kwa neema ya kawaida inayosaidia kutenda); kumbe pengine, nikiwa nimezama katika somo gumu, ghafla napata wazo la kusali ama kwa kuelewa somo hilo ama kwa kumuombea mtu. Katika mfano wa kwanza busara ndiyo iliyoniongoza kutekeleza imani na ibada; katika ule wa pili ni uvuvio maalumu wa Roho Mtakatifu ulionielekeza kabla sijafikiria. Jambo hilo ni jipya, ingawa kuvuka kunafanyika pengine polepole na pengine kwa kasi au hata ghafla.
Hapa ni lazima tuzingatie vipaji si kwa jumla na kinadharia tu, bali kinaganaga na kimatendo, vilivyofafanuliwa na walimu wa Kiroho. Kipaji cha elimu ndicho chanzo cha mang’amuzi ya ubatili wa malimwengu kulingana na mambo ya Kimungu, na hasa cha ujuzi wa uzito wa dhambi ya mauti unaomfanya mtu aiogope kweli. Kusoma kwa makini vitabu vya dini na kujitafiti dhamiri kusingetosha kamwe kutia majuto ya namna hiyo yanayoonyesha uvuvio maalumu, jambo jipya kweli.
Vilevile kipaji cha ibada ndicho chanzo cha utashi kutawaliwa na uwemo mtamu wa Mungu katika sala ya utulivu: “Mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, ‘Aba!’ yaani, ‘Baba!’ Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu” (Rom 8:15-16). Roho Mtakatifu anatoa ushahidi huo kwa kututia upendo wa kitoto kwa Mungu tusioufikia kwa msaada wa neema za kawaida. Tena kipaji cha ibada kinaeleza maneno haya: “Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa” (Rom 8:26).
Hatimaye kipaji cha hekima ndicho chanzo cha kung’amua uwemo wa Mungu ndani mwetu kwa kutegemea kwa pamoja uvuvio maalumu na ulinganifu wetu na mambo ya Kimungu unaotokana na upendo. Huo uvuvio unatumia ulinganifu huo kwa kuutekeleza (tendo la kumiminiwa la upendo) ili kutuonyesha jinsi mafumbo ya imani yanavyotimiza matamanio yetu ya juu zaidi na kuchochea mengine mapya. Hapo tendo ni la kumiminiwa si kwa sababu linatokana na maadili ya kumiminiwa bali kwa sababu lisingepatikana pasipo uvuvio maalumu ambao vipaji vinatuweka tayari kuupokea; linahitaji neema inayotenda, si ile ya kawaida tu inayosaidia kutenda.
Kadiri ya maelezo hayo, tofauti kati ya vipaji na maadili si ya kiwango tu: mwenendo si uleule ukiwa na uvuvio maalumu au la. Tofauti hiyo ni wazi pale ambapo tendo la busara katika kuamua la kufanya linafuatwa na lingine la kipaji cha shauri lisilotegemea mifuatano ya mawazo bali uvuvio maalumu unaofanya busara yenye kusitasita isitumike tena wakati huo. Lakini pengine uvuvio huo unarahisisha tu uamuzi wa busara kwa kukumbusha neno fulani la Injili: hapo tofauti si wazi. Vivyo hivyo katika mfano wa umwagiliaji wa bustani, tofauti inajitokeza wazi mtu akivuka mara toka namna ya kwanza hadi ya nne; lakini badiliko linaweza likatokea hatua kwa hatua.
Ili kueleza sala ya kumiminiwa hakuna haja ya kudai inafanyika kwa mawazo ya kumiminiwa kama yale ya malaika, bali unatosha ule mwanga wa kumiminiwa unaostawi daima katika mwadilifu yeyote mwenye upendo kwa msalaba na usikivu kwa mlezi wa ndani. Kwa namna hiyo imani inazidi kupenya na kuonja.
Vilevile hakuna haja ya kudai uwepo mwanga wa kinabii, kwa kuwa ule wa vipaji unatosha: “Katika sala ya kumiminiwa Mungu anatazamwa kwa mwanga wa hekima ambao unainua roho itambue mambo ya Mungu, ingawa umungu wenyewe hauonekani moja kwa moja. Ndivyo kwa neema Mungu anavyoonekana na mwanasala baada ya dhambi asili, ingawa kwa ukamilifu mpungufu kuliko katika utakatifu asili” (Thoma wa Akwino). Yaliyo mapya katika sala ya kumiminiwa yanaelezwa vya kutosha na mafundisho ya mapokeo. Thibitisho ni kwamba neema ya maadili na vipaji inayotuunganisha na Mungu, ni bora kuliko karama zinazotuwezesha tu kujua au kupendekeza ishara za utendaji wake. Muungano wa dhati na Mungu aliyemo mwetu unapita ishara hizo ambazo zinaulenga tu; tena kuzijali mno kunasogeza mbali na sala ya kumiminiwa inayomfikia Mungu mwenyewe katika giza la imani.
Kwa kawaida wanaoshikilia mafundisho hayo ni wale waliomiminiwa sala, kumbe wanaoyapinga wengi wao wanakiri hawana mang’amuzi hayo, ila wanajaribu kujichorea kadiri ya masomo yao wakijiuliza kuhusu maana ya maneno ya walimu wa Kiroho, k.mf. kumuona Mungu. Bila shaka si kumuona moja kwa moja alivyo, bali ni aina ya ujuzi inayofanana na mang’amuzi kumhusu Mungu kwa njia ya upendo wa kumiminiwa anaotuvutia kwake. “Kuonja kwa imani” ndio tokeo maalumu la kipaji cha hekima: “Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema” (Zab 34:8). Walimu hao wametuachia mafundisho ambayo hatujaelewa kikamilifu. Ili tuweze kuyaboresha tunahitaji mang’amuzi ya juu pamoja na ujuzi wa dhati wa teolojia; lakini haitoshi tujipangie maendeleo hayo, mpaka tujaliwe: kabla ya hapo tupenye zaidi maneno yao tusiyapotoshe.
Je, wanaoishi Kiroho wanaitwa wote kwa jumla na kwa mbali kumiminiwa sala? Tunajibu “ndiyo” kwa kufuata mafundisho juu ya vipaji vya Roho Mtakatifu wanavyojaliwa waadilifu wote, na juu ya matakaso ya Kimungu yanayohitajika kufikia ukamilifu wa Kikristo unaotupasa wote kuulenga. Sababu kuu za jibu hilo ni tatu, nazo zinahusu mzizi, maendeleo na lengo la maisha ya Kiroho.
Sababu ya kwanza: mzizi wa kumiminiwa sala ni uleule wa maisha ya Kiroho ya kawaida, yaani neema ya maadili na vipaji. Basi, kwa kawaida usikivu kwa Roho Mtakatifu kadiri ya namna ipitayo maumbile ya vipaji unatakiwa kuja kumtawala mtu anayeendelea, ili ufidie upungufu wa kudumu wa namna ya kibinadamu ya maadili na ya utendaji wetu ukisaidiwa na neema za kawaida. Basi, maisha ya kuzama katika mafumbo, ambayo sifa zake maalumu ni huo usikivu na hiyo namna ipitayo maumbile ya kumiminiwa ujuzi wenye upendo, kwa kawaida yanajitokeza kwanza katika hatua ya mwanga, halafu hasa katika ile ya muungano.
Sababu ya pili: katika maendeleo ya maisha ya Kiroho utakaso haukamiliki pasipo matakaso ya Kimungu, ambayo yamo upande wa mafumbo, kwa kuwa sala ya kumiminiwa inaanza na takaso la Kimungu la hisi, halafu inapanda juu katika usiku wa roho. Hapo Roho Mtakatifu anatakasa unyenyekevu na maadili ya Kimungu akitokeza sababu za Kimungu za maadili hayo, yaani ukweli mkuu unaojifunua, huruma yenye enzi zote inayosaidia, na wema wa kupendeza kupita yote. Basi, matakaso hayo ni sehemu za njia ya kawaida ya utakatifu na yanawaondolea haja ya kupitia toharani wale wanaoyavumilia kwa moyo. “Ni lazima kupitia usiku wenye giza wa kutakaswa ili kuja kukamilika” katika muungano unaotugeuza ambapo “hakika mtu hasumbuliwi tena na shetani, ulimwengu, mwili na tamaa; hata anaweza kukariri maneno ya Wimbo ulio Bor (2:11-12), ‘Kaskazi imepita, masika imekwisha, imekwenda zake; maua yatokea katika nchi’” (Yohane wa Msalaba).
Sababu ya tatu: lengo la maisha ya Kiroho ni lilelile la maisha ya mafumbo, yaani heri ya kumuona Mungu milele, na upendo wa kudumu unaotokana nayo. Basi, maisha ya kuzama katika mafumbo yanasogeza karibu zaidi na lengo hilo kuu, ni kama utangulizi wake, inavyothibitishwa na heri, zilizo matendo bora yatokanayo na maadili na vipaji. Hivyo maisha ya mafumbo, ambayo sifa yake maalumu ni kumiminiwa na Mungu tendo la kumjua na kumpenda, yanaonekana tena sehemu ya njia ya kawaida ya utakatifu. “Sala takatifu ya kumiminiwa ndiyo lengo lenyewe la mazoezi yote ya Kiroho” (Fransisko wa Sales). “Ni kosa letu tu tusipoonja kamwe utamu usiosemekana wa kumiminiwa sala” (Y. Alvarez de Paz).
Mafundisho hayo yanatuelekeza kukiri kwamba wanaoishi Kiroho wanaitwa wote kwa jumla na kwa mbali kumiminiwa sala. “Lakini nawaungamia kuwa wachache sana kati yetu wanajiandaa kumuona Bwana, kuvumbua lulu azizi tunayozungumzia… Lo! Jinsi tunavyohitaji kukomesha ulegevu wowote tulionao” (Teresa wa Yesu). Wasiwasi kuhusu wito wa binafsi na wa karibu wa kumiminiwa sala unatokana na kwamba “watu wengi wanakataa kuvumilia ukavu na ufishaji hata uwe mdogo namna gani, badala ya kutenda kwa subira isiyoshindikana. Hapo Mungu haendelei kuwatakasa kwa dhati” (Yohane wa Msalaba). Hakika, si waadilifu wote wanaitwa binafsi na kwa karibu wamiminiwe sala kwa kuwa dalili tatu za wito huo hazipatikani ndani yao wote. Hatimaye wito unaweza kuwa wa kutosha na hata hivyo usizae kutokana na ulegevu wetu; kinyume chake unaweza kuwa wa hakika kwa kiasi mbalimbali, hata kutufikisha ama kwenye ngazi za chini ama kwenye zile za juu za sala ya kumiminiwa.
Kutokana na hayo, hamu ya kumiminiwa sala ni halali kwa wote, mradi wabaki wanyenyekevu na kumuachia Mungu apange wakati wa kuwajalia. Kwa mkulima ni halali kutamani na kuomba mvua itakayootesha mbegu alizozipanda, mradi ayaachie maongozi ya Mungu. Ikiwa sala yoyote inatakiwa kuwa kwa pamoja nyenyekevu, yenye tumaini na udumifu, ni hivyo pia kwa ile tunayoomba ujuzi hai na wa dhati zaidi wa mafumbo tuliyofumbuliwa: Maandiko matakatifu yana sala hiyo sehemu mbalimbali.
Kabla dalili yoyote haijaonyesha wito wa karibu wa mtu kumiminiwa sala, tuwajulishe wote ukuu wa roho ya imani inayotufanya tutazame upande wa Mungu mafumbo, ibada, watu na matukio. Kwa kuwa mtazamo huo unakuwa kamili na wa kudumu kwa kumiminiwa sala tu, tunasema juu ya neema hiyo bila kuitaja bado, ili mtu yeyote atamani na kujiombea imani yenye kupenya na kuonja mafumbo ya wokovu. Kama tunavyofanya mtu atamani uzima wa milele kabla hajaonyesha dalili za uteule wake, inafaa atamani yale yote yaliyo sehemu za njia ya kawaida ya kuufikia uzima huo.
Ila tutofautishe nia na utekelezaji wake. Upande wa nia, lengo linatangulia njia; kumbe upande wa utekelezaji tunatakiwa kupanda taratibu toka chini hadi juu, na kukwepa haraka, la sivyo tutaharibu kila kitu, kama mtu anayetaka kupaua kabla hajaweka misingi, au kuruka kabla hajaota mabawa. Kwa hiyo ni lazima tukumbushe mfululizo masharti ya muungano halisi na Mungu: kujikusanya karibu daima, kujinyima kikamilifu, kuwa na moyo safi, unyenyekevu wa kweli, udumifu katika sala hata katika ukavu wa muda mrefu, na upendo mkubwa wa kidugu. Tukiongeza upendo kwa liturujia na kwa mafundisho ya imani tunajiandaa kweli kuitwa kwa karibu kwenye urafiki wa ndani na Mungu.
Wito huo unapokuja kuonekana inafaa wahusika wasome juu ya dalili zake tatu wasije wakapotoshwa na tabu na ukavu wa usiku wa hisi. Wakimiminiwa sala mara nyingi waendelee kusoma maandishi ya namna hiyo, hasa yale yanayoangalisha dhidi ya hamu ya neema za pekee (njozi, mafunuo n.k.). Wakilegea kidogo, tuwaambie mara juu ya kasoro za wanaoendelea, juu ya kupenda msalaba, juu ya haja ya kutakata kwa dhati zaidi ili kuungana kwa ndani na Mungu.
Kwa hakika watakatifu wanapatwa na maradhi kama watu wengine; suala ni kujua kama, mbali ya maradhi ya mwili, wana afya na msimamo mzuri upande wa nafsi. Utakatifu na kuzama katika mafumbo vinaweza vikaendana na maradhi ya nafsi kiasi tu, maana yale ya kudumu hayapatani na hali ya juu ya maisha ya Kiroho.
Kama walivyokwishafanya wanasaikolojia na wanateolojia wengi, tutazingatia tofauti zilizopo: 1) upande wa wahusika; 2) upande wa matukio; 3) upande wa matokeo.
“Wagonjwa wengi wa umanyeto wana hali ya akili ya pekee inayotambulikana kwa urahisi. Tangu utotoni wenye elekeo hilo wanagundulika kwa sifa za pekee. Kwa kawaida ni wasichana wenye akili kubwa, wenye kukomaa mapema mno, wepesi kushtuka, wenye majivuno, wanaojaribu kujivutia macho ya watu, werevu katika kudanganya na kuongopa, na wanaopatwa na hofu za usiku, ndoto na majinamizi. Umanyeto ukishathibitishwa, hali ya nafsi na ya maadili ya wagonjwa hao sifa yake kuu upande wa akili ni ugeugeu mkubwa mno unaowafanya wasidumu katika lolote… hawawezi kabisa kumaliza jambo la maana. Pamoja na hayo wana elekeo la wazi la kupinga, la kubishana, la kuwa na mawazo ya ajabuajabu… na vilevile la kuiga, kudanganyika na kujidanganya. Upande wa maadili hali ni hiyohiyo: tabia isiyotabirika, kaidi, bunifu, geugeu kupita kiasi… undumakuwili, uongo, wepesi wa kuigiza, kudanganya na kubuni: elekeo la kutenda ghafla na wakati usiofaa maovu makubwa au matendo bora ya kushangaza; haja ya kudumu ya kujitokeza, n.k.” (E. Régis). Halafu wana mawazo yasiyobanduka kwa ndani, njozi bandia, kuchanganyikiwa na hatimaye kichaa. Hivyo tunaweza kuona ugonjwa wa nafsi unavyozidi kustawi, akili inavyozidi kushindwa kuongoza mwenendo, kumbukumbu inavyozidi kusambaratika hata kumfanya mgonjwa ajione ana pande mbili; mapema rohoni yanabaki tu mawazo machache yasiyobanduka. Pamoja na akili, utashi unapungua vilevile: miguso inakuja kutawala pamoja na ugeugeu.
Kinyume chake, akili ya wale ambao wanazama katika mafumbo na kutoka nje ya nafsi, inapanuka kwa kumjua Mungu, sifa zake na kweli za iman,i na vilevile kwa kujifahamu kwa dhati. Hao wanasema kuwa kwa nukta chache za kuzama katika mafumbo wanajaliwa kujifunza mengi kuliko kwa kusoma vitabu vingi. Katika nafasi za namna hiyo wanapokea mwanga wa juu unaowafanya wachungulie yale yote waliyokwishayajua kama kwa muhtasari bora, hai, mwangavu, unaochochea utashi ujitahidi kutenda makuu kwa udumifu wa ajabu, bila kujali matatizo yasiyosemekana. Pamoja na hayo, watu hao ni wanyenyekevu na watiifu kwa matakwa ya Mungu hata katika majaribu makali. Ndani mwao tunaona fungamano na ulinganifu kati ya maadili tofauti, na juu ya yote upendo wa Mungu na wa jirani na busara vinavyowapatia amani na utulivu wa ajabu. Kinyume cha mahangaiko na ugeugeu wa wenye umanyeto, wanafanya kazi ili kutimiza jambo gumu, wakidumu kutenda mema, kujali ukweli na kutunza siri.
Tofauti kati ya hali halisi ya kutoka nje ya nafsi na ile ya umanyeto ni kubwa vilevile. Ili tupate hakika ya kwamba hazifanani hata kidogo inatosha tuishuhudie hiyo ya mwisho mara moja au mbili.
Katika matukio yaliyotokana na ugonjwa mtu anachanganyikiwa kwa kuona mambo ambayo hayapo, au kufuata kumbukumbu au kujisimulia, kadiri ya kiwango cha ndoto. Hatua ya kwanza inafanana kidogo na tatizo la kifafa, isipokuwa kwa kuhisi aina ya mpira ikipanda kooni; ni hisi ya kukabwa inayosababishwa na koo kuvimba. Hatua ya pili inaleta vitendo vya fujofujo na kunyonganyonga mwili mzima. Hatua ya tatu inaleta pozi za hofu, wivu, tamaa chafu kuhusiana na taswira inayomchanganya mtu. Hatimaye huyo anapatwa na kulia au kucheka; ndio mwisho wa tatizo, unaofuatwa na uchovu mkubwa.
Kumbe, hali halisi ya kutoka nje ya nafsi ina utulivu wa roho iliyounganika na Mungu kwa dhati unaotokana na neema ya kukusanyika kwa ndani ambayo Mungu tu anaweza kujalia na inapita yale yote yanayotokana na juhudi za kujikusanya. Ni elekeo la utu mzima, roho na mwili, kwa jambo la Kimungu lililotokea katika ubunifu au katika akili. Mwisho wa hali hiyo ni kurudia ile ya kawaida kwa utulivu tu, pamoja na sikitiko la kutoona tena njozi hiyo na furaha ya Kiroho iliyotokana nayo. Tena hali hiyo, badala ya kudhoofisha mwili, inauongezea nguvu mpya.
Tofauti hizo ni kubwa zaidi. Wagonjwa wa umanyeto wanaendelea kuchanganyikiwa na kuzidisha udanganyifu, uongo, unyama na uzinifu hata ugeugeu wa hisi unakuja kutawala akili na utashi moja kwa moja. Nafsi inasambaratika na fujo ya ndani inaelekea kichaa. Kinyume chake hali halisi ya kutoka nje ya nafsi ina ustawi mkubwa zaidi na zaidi wa ujuzi wa mambo ya Mungu, wa maisha ya Kiroho, wa wokovu na upotevu wa watu, pamoja na ustawi wa kudumu wa upendo kwa Mungu na wa kujitoa kwa jirani, inavyoonyeshwa na miundo ambayo wanaianzisha na mara nyingi wanaifanikisha kiasi kwamba inadumu karne na karne.
Wenye umanyeto wanatawaliwa na wazo moja tu (k.mf. lile la kujiua) kwa kupotewa na mengine yote. Kumbe wanaozama katika mafumbo wazo ambalo linatawala mengine na kuyalinganisha kikamilifu ni wazo la Mungu, la wema wake usio na mipaka kwetu, pamoja na hakika angavu na ya dhati ya kwamba inatupasa kuitikia upendo wake. Hakuna kusambaratika kwa nafsi, bali sehemu zake zinajipanga kadiri ya utaratibu wa upendo: kwanza Mungu ambaye apendwe kuliko vyote, halafu watu ambao waokolewe. Ndiyo sababu watakatifu wana kipawa cha kupanga mambo hata kibinadamu, kama walivyokiri wanasaikolojia kadhaa wasio na imani, k.mf. M. wa Montmorand, “Wana kipawa cha kupanga na cha kuongoza na wanaonekana wenye elekeo zuri upande wa uchumi. Miundo wanayoianzisha ni hai na inadumu; katika kuwaza na kuendesha mipango yao wanaonyesha busara na ushujaa”.
Katika maisha ya waliozama katika mafumbo tukio fulani linaweza likaleta dhana ya kuwepo umanyeto. Hapo ni lazima kuchunguza kwanza hali ya mwili na maadili ya mhusika. Kiongozi wa Kiroho anaweza (na pengine anapaswa) kushauriana na daktari. Mara nyingi uchunguzi wa makini utaleta hakika fulani, hasa ukiendana na kusali, kutojitafutia faida, na kulenga ukweli kwa nia safi.
Ya Kiorthodoksi
Ya Ukristo wa Magharibi
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Sala ya kumiminiwa kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |