Ukristo na dini nyingine

Watu wa dini mbalimbali waliokusanyika huko Assisi kwa Siku ya Kimataifa ya Nne ya Sala kwa ajili ya Amani, tarehe 27 Oktoba 2011.


Ukristo na dini nyingine zinahusiana kwa kiasi tofauti, kadiri ya mazingira asili, historia, mafundisho kuhusu imani na maadili, desturi, ibada n.k.

Ukristo na Uyahudi

[hariri | hariri chanzo]

Ni wazi kuwa Ukristo unahusiana zaidi na dini ya Uyahudi, kwa sababu unatokana nayo na kutumia vitabu vyake vitakatifu (Tanakh na pengine Deuterokanoni pia). Haiwezekani kumuelewa Yesu kwa kumweka nje ya mazingira ya Kiyahudi.

Dini hizo mbili zilitengana moja kwa moja miaka 50 hivi baada ya Yesu kuaga dunia. Ni kwamba Wayahudi wa shule ya Jabneh (mwaka 80 hivi B.K.) waliamua kuwatenga kama wazushi wananchi wenzao waliomuamini Yesu Kristo, hasa baada ya kuona hawakusaidia vita vya ukombozi dhidi ya wakoloni Warumi vilivyosababisha maangamizi ya Hekalu la pili na mji wa Yerusalemu mwaka 70 B.K.

Tangu hapo Wakristo hawakushiriki tena ibada pamoja na Wayahudi, wakazidi kuzingatia sakramenti ya Kumega Mkate katika Siku ya Bwana (Jumapili, siku inaposadikika Yesu alifufuka) badala ya Sabato (Jumamosi, siku ya pumziko ya Wayahudi). Kabla ya hapo Wakristo wa Kiyahudi walikuwa wanashika siku zote mbili.

Ukristo na Ubuddha

[hariri | hariri chanzo]

Hakuna uhusiano wa kihistoria kati ya Yesu na Ubuddha. Hata hivyo mambo kadhaa yanafanana.

Yesu alifundisha kuhusu nidhamu mbili zinazompelekea mtu kuwa mwadilifu na hatimaye kuurithi utukufu wa kiroho ambao karama yake ni uzima wa milele: hizo ni kumpenda Mungu kwa moyo wako wote na kwa akili yako yote na kwa nguvu zako zote, na jirani yeyote kama unavyojipenda mwenyewe.

Buddha alifundisha hali ya kutodhuru viumbe hai wowote, tena kuwa na moyo mkuu wa mapenzi kwa vitu vyote. Hii ni miongozo inayolenga mtu atambue tabu anazodumisha yeye mwenyewe, kwa matendo yake na upeo ulio na mipaka, katika maisha yake ya kila siku.

Baada ya hili, mafundisho ya Kristo yanatofautiana katika kuchukulia hali hii. Kwa mujibu wa Kristo, dhambi, matendo yenye kukosea kanuni za kiroho na hata za kimaumbile, hufutwa na toba; wakati katika mafundisho ya Buddha, makosa yote yanatokana na kutokuwa makini. Hivyo, kwa mujibu wa Buddha, njia pekee ya kumkomboa mtu na shida zake ni kufuata mwongozo wa Nguzo Nane ambazo humweka katika hali ya kuweza kuamka kiroho wakati utulivu wa kimwili na wa kiakili unapofikiwa. Haya ndiyo yanayofanya Ubuddha kuwa ni njia inayojali sana nidhamu ya mtu kimatendo, wakati Ukristo hufuata sana moyo wenye kukiri makosa, na kutafuta uadilifu wa kweli wa kiroho. Huu ni uzuri wa pekee kutoka kwenye mafundisho ya Yesu: Tubuni kwa kuwa saa ya ukombozi ni sasa...

Jingine lenye tofauti ni kuwa Kristo hufundisha kuhusu Upendo kwamba ni Mungu, kwa kuwa Upendo una maana kuliko elimu yote ya binadamu, nao ndio unaounganisha na kutunza vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Hilo hutambulika kupitia Kristo ambaye hujidhihirisha kwa yule mwenye kumpokea Roho wa Mungu. Upande wa Buddha, hukanusha nafsi na pia Mungu, akisema: Ni Buddha mwenye ufahamu wa milele, tena hana nafsi isipokuwa Utupu; na ni wenye furaha isiyo kifani izidiyo yote yenye kufanyika ulimwenguni, yaani Nirvana; kila mtu ni Buddha aliyesahau asili yake ya ndani kabisa.

Ukristo na Uislamu

[hariri | hariri chanzo]

Ukristo na Uislamu vinafanana zaidi kwa sababu Muhammad alifahamu Wayahudi na Wakristo wengi katika nchi yake na katika safari zake. Dini hizo tatu zinajulikana kwa kushika imani katika Mungu Pekee, muumba wa vitu vyote, na kwa kumchukua Abrahamu kama kielelezo cha imani na rafiki wa Mungu.

Mafundisho ya msingi ya Uislamu ni unyenyekevu kwa Mola mmoja aitwaye Allah , mwingi wa rehema na mwingi wa fadhila; nguzo ya Uislamu ni kumuabudu. Katika Uislamu, unyenyekevu wa mtu katika kumcha Mola kwa ibada na swala humpa kukirimika na kuhifadhika kwa Mola wake mwenye fadhila, ambaye atamtunuku haki yake. Naye mnyenyekevu kwa Mola ataishi kuona utukufu mwingi wa Mola wenye kutajwa katika Kurani kwa majina 99 ya Allah. Kati ya sifa na utukufu huo ulio na majina mengi, baadhi yake ni Al Rahman (kwa Kiarabu, "Mwenye rehema"), Al Nur ("Mwenye nuru") n.k. Hayo hufanana na neno la Nuru ya Bwana, rehema na ukombozi kuwa utukufu wa Mbingu katika mwongozo wa Kikristo.

Pia Uislamu unafundisha udugu miongoni mwa Waislamu yaani mzizi wa neno linalotumika sana katika Kurani: Waly (Wala, Wilayat, Mawla, Awla) katika kueleza jinsi Mwislamu apasavyo kuishi karibu na mwenzake. Nalo husisitiza upendo na kulindana kwa heri na pia kuepushana na shari. Hilo linafanana na upendo ambao katika Ukristo ndio adili kuu kuliko yote:

Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo... mimi si kitu kabisa. (1 Wakorintho 13:1-11).

Lakini katika Ukristo upendo hauna mipaka wala masharti. Unatakiwa kuenea kwa maadui pia na kusamehe kila mara kufuatana na mfano wa Baba wa Mbinguni.

Mwislamu kadiri ya wingi wa unyenyekevu na usafi wa moyo wake huakisi sifa za Mola wake. Uislamu hufundisha kuhusu vita vya ndani ambavyo muumini hupigana na nafsi yake yenye matamanio ya chini, ambayo huzaa chuki, dhuluma, wivu na maovu mengine ili kuishinda kwa utukufu wa Mola na kudumisha dini (mwongozo) yake katika ngazi zote za maisha.

Kabla yake Yesu alihimiza wote wafuate mfano wake wa upole na unyenyekevu wa moyo, akitoa kielelezo katika Heri Nane za hotuba ya mlimani. Tofauti ya msingi ni kuwa kwa mujibu wa Kristo, ni kwa neema ya imani katika Neno la Uzima kwamba mtu hukombolewa kutoka matamanio yake ya kibinadamu, mbali ya kwamba anapaswa kujitahidi asije akapotewa na neema hiyo na kurudia utumwa wa dhambi.

Ni imani ya Wakristo na ya Waislamu kwamba Yesu atarudi duniani kwa utukufu, ingawa jambo hilo wanalitafsiri kwa namna tofauti.

  • Ankerl, Guy (2000) [2000]. Global communication without universal civilization. INU societal research. Juz. la Vol.1: Coexisting contemporary civilizations : Arabo-Muslim, Bharati, Chinese, and Western. Geneva: INU Press. ISBN 2-88155-004-5. {{cite book}}: |volume= has extra text (help)
  • Ingham, Michael, Bp. (1997). Mansions of the Spirit: the Gospel in a Multi-Faith World. Toronto, Ont.: Anglican Book Centre. ISBN 1-55126-185-5
  • Zuckermann, Ghil'ad (2006). "'Etymythological Othering' and the Power of 'Lexical Engineering' in Judaism, Islam and Christianity. A Socio-Philo(sopho)logical Perspective", Explorations in the Sociology of Language and Religion, edited by Tope Omoniyi and Joshua A. Fishman, Amsterdam: John Benjamins, pp. 237–258. ISBN 90-272-2710-1.
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ukristo na dini nyingine kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.